Wananchi Same Mashar...
Wananchi Same Mashariki watakiwa kujiandaa mapema kukabiliana na athari za EL Nino
01 Oct, 2026
Wananchi Same Mashariki watakiwa kujiandaa mapema kukabiliana na athari za EL Nino

Wananchi Same Mashariki watakiwa kujiandaa mapema kukabiliana na athari za EL Nino

📍Ndungu, Same.

Wananchi wa Jimbo la Same Mashariki, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari na kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu.

Tahadhari hiyo imetolewa kutokana na uwezekano wa kutokea kwa mafuriko, mmomonyoko wa udongo, kupasuka kwa ardhi pamoja na changamoto nyingine zinazoweza kuhatarisha maisha na mali za wananchi.

Rai hiyo imetolewa katika semina maalumu iliyolenga kutoa elimu kuhusu El Niño, athari zake kwa jamii pamoja na hatua muhimu za kuchukua kabla, wakati na baada ya mvua hizo. Semina hiyo imeandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Mhe. Anne Kilango Malecela, na kuwakutanisha Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Madiwani pamoja na wataalamu kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Akizungumza katika semina hiyo, Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Mhe. Anne Kilango Malecela, ameishukuru GST kwa kutoa elimu hiyo na kusisitiza umuhimu wa taarifa za tahadhari kuwafikia wananchi kwa wakati.

Amesema atahakikisha elimu na taarifa zinazohusiana na El Niño zinaendelea kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, ili kuwawezesha kuchukua hatua stahiki za kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza.

Kwa upande wake, Mjiolojia Mwandamizi kutoka GST, Gabriel Mbogoni, amesema maeneo mbalimbali yaliyotembelewa na wataalamu katika Wilaya ya Same yanakabiliwa na changamoto zinazofanana, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kuchukua tahadhari, hususan katika maeneo yaliyo katika hatari ya mafuriko na mmomonyoko wa udongo.

Mbogoni amesema baadhi ya shughuli za kilimo zinazofanyika katika maeneo hatarishi zinaweza kuchangia mmomonyoko wa udongo na kupasuka kwa ardhi, hali inayoweza kuongeza madhara wakati wa mvua kubwa, ikiwemo kipindi cha mvua za El Niño.

Aidha, semina hiyo imeambatana na ziara ya kutembelea eneo hatarishi la Mto Saseni, Kata ya Kihurio, ambapo wataalamu walibaini kuwa mto huo umeacha njia yake ya asili.

Kutokana na hali hiyo, GST imeshauri mto huo kurejeshwa katika njia yake ya asili ili kupunguza uwezekano wa kutokea kwa madhara kwa wananchi na mali zao, hususan iwapo kutanyesha mvua kubwa kwa wingi.

Ushauri huo umetolewa wakati mamlaka za hali ya hewa zikiendelea kutoa taarifa na tahadhari kuhusu mwenendo wa mvua zinazotarajiwa katika maeneo mbalimbali nchini, huku wananchi wakihimizwa kuzingatia taarifa rasmi na kuchukua hatua za tahadhari mapema.