Waziri Mkuu Dkt. Mwi...
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Atembelea Banda la GST Kufunga Maonyesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini Geita
06 Oct, 2026
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Atembelea Banda la GST Kufunga Maonyesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini Geita

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Atembelea Banda la GST Kufunga Maonyesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini Geita

GEITA, Oktoba 3, 2026

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ametembelea banda la Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) wakati wa hafla ya kufunga Maonyesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkoani Geita.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amepata fursa ya kufahamishwa kuhusu shughuli, tafiti na huduma mbalimbali za kitaalamu zinazotolewa na GST, hususan tafiti za madini na jiosayansi zinazolenga kuongeza uelewa kuhusu rasilimali za madini zilizopo nchini.

Maelezo hayo yametolewa na Kamishna wa Madini nchini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, ambaye alieleza namna tafiti zinazofanywa na GST zinavyosaidia kuzalisha taarifa muhimu za kitaalamu kuhusu rasilimali za madini, kutambua maeneo yenye uwezekano wa kuwa na madini na kuchochea uwekezaji katika Sekta ya Madini.

Aidha, Waziri Mkuu ameelezwa kuhusu tafiti mbalimbali za jiosayansi zilizofanyika nchini na umuhimu wa taarifa hizo katika kubaini, kutathmini na kuelewa vizuri rasilimali za madini. Taarifa hizo ni muhimu kwa Serikali, wawekezaji na wachimbaji katika kufanya maamuzi sahihi kuhusu shughuli za utafutaji, uchimbaji na uwekezaji katika Sekta ya Madini.

Akizungumza katika hafla ya kufunga maonyesho hayo, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kutenga asilimia 10 ya makusanyo ya Sekta ya Madini kwa ajili ya kugharamia tafiti za madini nchini.

Mhe. Mavunde amesema uwezeshaji huo utaipa GST uwezo wa kuongeza wigo wa tafiti katika maeneo mbalimbali nchini, hatua ambayo itasaidia kuongeza upatikanaji wa taarifa sahihi na za kitaalamu kuhusu rasilimali za madini.

Amesema taarifa hizo zitakuwa na manufaa makubwa kwa wachimbaji, hususan wachimbaji wadogo, kwa kuwa zitawasaidia kuelewa zaidi maeneo yenye uwezekano wa kuwa na rasilimali za madini na hivyo kupunguza changamoto za kufanya shughuli za uchimbaji bila kuwa na taarifa za kutosha za kitaalamu.

“Kuanzia tarehe 1 Julai 2026, Serikali imeanza kutenga asilimia 10 ya makusanyo ya Sekta ya Madini kwa ajili ya kugharamia tafiti za madini nchini, hatua inayolenga kuongeza utafiti na upatikanaji wa taarifa za rasilimali za madini,” amesema Mhe. Mavunde.

Kwa upande wake, GST inaendelea kusisitiza umuhimu wa tafiti za jiosayansi katika kuwezesha matumizi sahihi na endelevu ya rasilimali za nchi. Tafiti hizo pia hutoa msingi wa taarifa zinazoweza kutumika katika kupanga shughuli za uchumi, kuendeleza sekta ya madini na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Uwekezaji zaidi katika tafiti za madini unatarajiwa kuongeza wigo wa taarifa za kijiolojia nchini, kuwezesha ugunduzi wa maeneo mapya yenye uwezekano wa kuwa na madini na kuongeza fursa kwa wananchi kushiriki katika shughuli za Sekta ya Madini.