Historia ya GST

 

Historia ya GST

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imetokana na Idara kongwe ya Madini iliyoitwa Geological Survey Department (GSD). Idara hii ilianzishwa Mwaka 1925 na Mamlaka ya Utawala wa Makoloni ya Serikali ya Kikoloni ya Mwingereza (British Overseas Management Authority- BOMA). Mkurugenzi wa kwanza wa GSD alikuwa Dr. E.O. Teale (1925-1936) na makao makuu ya GSD yalikuwa Dodoma. 

GSD ilianzishwa ili kuharakisha ukuaji wa Sekta ya Madini katika Koloni la Waingereza la Tanganyika na kazi kuu zilikuwa ni upimaji na uchoraji wa ramani za jiolojia pamoja na utafiti wa madini. Pamoja na kuwepo mabadiliko mbalimbali ya kiutawala katika kipindi cha ukoloni na baada ya uhuru wa Tanzania bado majukumu ya idara hii yaliendelea kubaki vilevile.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000 Serikali ilianzisha mchakato  wa uanzishaji wa Wakala za Serikali na ilipofika mwezi Disemba, 2005, Wakala wa Jiolojia Tanzania ulianzishwa kwa Sheria ya Wakala wa Serikali Namba 30 ya 1997 [CAP. 245] kama ilivyorekebishwa na Sheria Na.14 ya Mwaka 2009 chini ya iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini.

Uamuzi wa Serikali wa kuifanya GST kuwa Wakala ulilenga kupunguza ukubwa wa Serikali na kuongeza ubora na ufanisi wa kazi za jionsayansi na kuvutia wawekezaji katika Sekta ya Madini kutoka ndani na nje ya nchi. Matokeo ya mabadiliko hayo ya kisheria na kisera, uwekezaji katika Sekta ya Madini uliongezeka kwa kiwango kikubwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 ambapo kampuni za utafutaji na uchimbaji madini ziliongezeka. Kuongezeka kwa uwekezaji katika Sekta ya Madini kulisababisha pia kuwepo kwa ongezeko la mahitaji ya taarifa za jiosayansi ambazo ni muhimu katika kujua maeneo yenye uwezekano wa kuwepo kwa madini. 

Mwezi Julai, 2017 Serikali ya Tanzania ilifanya Marekebisho kwenye Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kupitia the Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, No. 7 ya Mwaka 2017. Kufuatia Marekebisho hayo, Muundo wa GST ulifanyiwa marekebisho yaliyopelekea kuundwa kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania na kuongezewa majukumu mapya.