GST kufanya utafiti...
GST kufanya utafiti wa eneo la ekari 157,192 kubaini mwendelezo wa mkondo wa madini ya Tanzanite
11 Nov, 2026
GST kufanya utafiti wa eneo la ekari 157,192 kubaini mwendelezo wa mkondo wa madini ya Tanzanite

GST kufanya utafiti wa eneo la ekari 157,192 kubaini mwendelezo wa mkondo wa madini ya Tanzanite

  Lengo ni kuongeza uzalishaji wa madini ya Tanzanite

▪️Utafiti kugusa eneo la nje ya ukuta wa eneo tengefu la Mirerani

▪️Wachimbaji wa Mirerani wamshukuru Rais Samia kwa mkakati wa kukuza biashara ya Madini

▪️GST yaelekezwa kukamilisha utafiti eneo la Lemshuku kuongeza uzalishaji wa Green Garnet na Tsavorite


📍Mirerani, Manyara.

Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imezindua rasmi mpango wa kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia kwa kutumia teknolojia za kisasa, zikiwemo ndege maalumu zisizo na rubani (Drone), ndege za utafiti zinazoruka karibu na uso wa dunia pamoja na vifaa vingine vya kisasa, kwa lengo la kubaini maeneo yenye viashiria vya uwepo wa madini nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, wakati wa hafla ya uzinduzi wa utafiti wa kubaini mwendelezo wa mkondo wenye madini ya Tanzanite katika eneo tengefu la Mirerani, iliyofanyika leo Novemba 09, 2026.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mavunde amesema kuwa hadi sasa ni asilimia 16 pekee ya eneo la Tanzania lililofanyiwa utafiti wa kina wa kijiolojia, huku asilimia 84 iliyobaki, sawa na takribani ekari milioni 233, ikiwa bado haijafanyiwa utafiti wa kina.

Ameeleza kuwa katika hatua ya kuongeza wigo wa tafiti hizo, Serikali inatarajia kufanya utafiti katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 160,772, sawa na asilimia 18 ya eneo la nchi, kupitia ushirikiano na wataalamu kutoka Hispania. Maeneo mengine yatakayofanyiwa utafiti ni Kigoma, Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Lindi na Mtwara, huku utafiti mwingine ukihusisha maeneo ya Dodoma, Singida, Tabora hadi Shinyanga.

Aidha, Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa Serikali imeanza kutenga asilimia 10 ya mapato yanayokusanywa katika sekta ya madini kwa ajili ya kugharamia tafiti za kina za kijiolojia. Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata taarifa sahihi kuhusu maeneo yenye madini na kupunguza uchimbaji wa kubahatisha unaosababisha upotevu wa muda na mitaji.

Naye, Mtendaji Mkuu wa GST, Mhandisi Ally Samaje, amesema kuwa lengo kuu la utafiti huo ni kuongeza uzalishaji wa madini ya Tanzanite kupitia upatikanaji wa taarifa za jiosayansi. Ameeleza kuwa utafiti huo unatekelezwa kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Madini pamoja na uchambuzi wa taarifa za kijiolojia ulioonesha uwepo wa maeneo yanayohitaji uchunguzi zaidi.

Ameongeza kuwa GST itatumia mbinu mbalimbali za kijiofizikia kubaini kwa usahihi wa miundo ya miamba yenye viashiria vya uwepo wa Tanzanite kabla ya hatua ya uchorongaji. Mbinu hiyo itasaidia Serikali na wachimbaji kupata taarifa sahihi za kisayansi kuhusu maeneo yenye matarajio ya kuwa na madini hayo.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, amesema kuwa utafiti huo utasaidia kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha kwa kubaini mashapo mapya ya madini ya Tanzanite katika eneo lote la uchimbaji.

Awali, akielezea utekelezaji wa utafiti huo, Meneja wa Uchoraji Ramani kutoka GST, Solomoni Maswi, amefafanua kuwa utafiti utafanyika kwa kutumia mikondo mitatu ya uchunguzi ambayo ni utafiti wa usumaku chini ya ardhi, utafiti wa umeme pamoja na utafiti unaohusisha mbinu za usumaku na umeme kwa pamoja, ili kubaini maeneo yenye viashiria vya madini.

Katika mpango huo, eneo la Mirerani limepewa kipaumbele maalumu, ambapo utafiti utafanyika ndani na nje ya eneo lenye ukuta kwa kutumia vifaa vya GST pamoja na mashine kubwa za uchorongaji zitakazowekwa katika eneo hilo hadi kukamilika kwa kazi iliyopangwa.

Utafiti huo katika eneo la Mirerani utahusisha eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 636, sawa na takribani ekari 157,192, ukiwa na lengo la kubaini maeneo mapya yenye viashiria vya madini na kutoa fursa za uchimbaji kwa vikundi vya wanawake, vijana na wananchi wengine wa Mirerani.

Vilevile, GST imeelekezwa kuendeleza utafiti katika eneo la Lemshuko, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara, ambako kumebainika viashiria vya madini ya vito, yakiwemo Green Garnet,Tsavorite na madini mengine.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya madini, wakiwemo wawakilishi wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini, Chama cha Wachimbaji wa Madini Wanawake (TAWOMA), Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (MAREMA), pamoja na watumishi wa Wizara ya Madini na taasisi zake