WAZIRI MKUU MAJALIWA Apongeza Mchango wa Sekta ya Madini Nchini.
Dar es salaam
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa aipongeza Wizara ya Madini katika juhudi mbalimbali inazofanya za kuiendeleza sekta ya madini kufikia asilimia 11.3 katika kuchangia kwenye Pato la Taifa.
Hayo, yamesemwa leo Novemba 19, 2023 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji Sekta ya Madini 2024 unaendelea katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Waziri Majaliwa amesema kuwa, uwepo wa Sera nzuri yenye ushawishi , mazingira salama yenye utulivu na amani ,uwepo wa masoko ya uhakika yaliyounganishwa na jiografia nzuri vyote hivyo vimekuwa vichocheo vikubwa katika ukuaji wa Sekta ya Madini nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa amefafanua kuwa , Serikali itaendelea kuboresha miundombinu yote inayohusiana na mnyororo mzima wa thamani madini ikiwa barabara , nishati ya umeme pamoja kuongeza idadi ya vituo vya mauzo na masoko ili kuiweka sekta katika hali ya ubora na ushindani.
Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu , Waziri wa Madini , Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa ili kuhakikisha nchi yetu inaendelea kunufaika na rasilimali madini, wizara imeendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za madini na kuhakikisha wananchi wananufaika na serikali inapata Mapato stahiki.
Akielezea kuhusu mwenendo wa ukusanyaji mapato Waziri Mavunde ameeleza kuwa, kiwango cha ukusanyaji maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 kwa mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.83 kwa mwaka 2023.
Kuhusu ukuaji wa sekta ya madini , Waziri Mavunde amefafanua kuwa, kwa mwaka 2021 ukuaji ulifikia asilimia 9.3 ambapo mwaka 2023 sekta ilikuwa kwa asilimia 11.3 na mchango wake katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 hadi 9.3.
Naye , Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge , Nishati na Madini ameipongeza Serikali kwa juhudi mbalimbali inazofanya hasa katika kuendeleza sekta ya madini nchini kwa ushirikiano na sekta binafisi ambayo inaleta maana halisi ya kaulimbiu ya Madini ni Maisha na Utajiri.
Meneja Mkazi Kampuni ya uchimbaji madini dhahabu ya Barrick Melkiory Ngido, amesema kuwa Kampuni Barrick inatambua mchango wa Serikali katika kuleta maendeleo hivyo ipo bega kwa bega katika kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa ambapo kwasasa kampuni inajenga Barabara yenye Urefu wa Kilomita 73 kiwango cha lami , pamoja na kiasi cha shilingi Bilioni 70 katika ujenzi wa madarasa 1200 na Mabweni 273.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa kampuni ya AngloGold Ashanti Simon Shayo amesema , kampuni ya GGM imeanza majadiliano na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuiuzia dhahabu pamoja na Mpango wa kutumia viwanda vya ndani vya kusafisha dhahabu.