GST Kuimarisha Mfumo wa Ufuatiliaji wa Mitetemo Nchini
GST Kuimarisha Mfumo wa Ufuatiliaji wa Mitetemo Nchini
📍Dodoma
Katika kuimarisha uwezo wa nchi katika kukabiliana na majanga ya asili ya jiolojia, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) itaendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za ufuatiliaji wa matetemeko ya ardhi pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.
Mpango huo ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vilivyobainishwa na Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kama alivyoeleza Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, wakati akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo. Alisema Serikali inalenga kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema ili kusaidia kulinda maisha ya wananchi, mali zao pamoja na miundombinu muhimu dhidi ya athari za majanga ya kijiolojia.
Katika utekelezaji wa jukumu hilo, GST itakusanya takwimu kutoka vituo vinne (4) vya kudumu vya kunakili mienendo ya mitetemo ya ardhi vilivyopo katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Geita na Mbeya. Takwimu hizo zitachakatwa na kutumika kuhuisha ramani ya vitovu vya matetemeko ya ardhi nchini, hatua itakayosaidia kuongeza uelewa kuhusu maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kutokea kwa mitetemo na kuwezesha mipango bora ya tahadhari na maandalizi ya kukabiliana na majanga hayo.
Aidha, GST itaendelea kufanya matengenezo na maboresho ya vifaa vya kisasa vya kunakili mitetemo ili kuhakikisha taarifa zinazokusanywa zinakuwa sahihi, za kuaminika na zinapatikana kwa wakati. Maboresho hayo yatasaidia kuimarisha uwezo wa wataalamu wa jiolojia kufanya uchambuzi wa kina kuhusu mwenendo wa matetemeko ya ardhi na kutoa taarifa muhimu kwa mamlaka husika na wananchi kwa wakati muafaka.
Sambamba na shughuli hizo, GST itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu njia bora za kujikinga au kupunguza athari za majanga ya asili ya jiolojia kupitia machapisho, semina, vipindi vya redio na televisheni pamoja na majukwaa mbalimbali ya habari. Elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu tahadhari muhimu zinazopaswa kuchukuliwa kabla, wakati na baada ya kutokea kwa matetemeko ya ardhi au majanga mengine ya kijiolojia.
Kupitia juhudi hizo, GST inaendelea kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanakuwa salama zaidi kwa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa majanga, kuongeza uelewa wa jamii na kuweka mazingira bora ya tahadhari ya mapema dhidi ya matetemeko ya ardhi nchini.

