GST, TFRA, na TFS Za...
GST, TFRA, na TFS Zasaini Hati ya Makubaliano Mkakati wa Kuzalisha Mbolea
30 Jan, 2024
GST, TFRA, na TFS Zasaini Hati ya Makubaliano Mkakati wa Kuzalisha Mbolea

Mbolea kuzalishwa nchini kwa kutumia Malighafi za ndani

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imesaini hati ya makubaliano (MoU) na TFRA pamoja na TFS ya Mkakati wa kuzalisha mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini.

Hafla ya utiaji saini imefanyika leo Januari 25, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Kilimo uliopo Jijini Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa GST, Kaimu Meneja wa Huduma za Jiolojia Bw. Maswi Solomon amesema, GST  imeingia kwenye makubaliano hayo kwa lengo la kutafiti na kubainisha maeneo yapatikanayo madini mbolea ili kuja na mkakati wa uzalishaji wa mbolea kwa kutumia malighafi zipatikanazo nchini.

Aidha, Bw. Maswi amesema, GST haiishii kwenye utafiti pekee ila pia kuainisha sehemu zinazopatika madini mbolea na kushauri nini kifanyike baada ya kugundua maeneo yapatikanayo malighafi hiyo.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni la mbolea (TFS) Samwel Mshote amesema, lengo la kusaini makubaliano hayo ni kuangalia ni kwa namna gani taasisi hizo zitashirikiana ili kupata malighafi kwa ajili ya kuzalisha mbolea kwa soko la ndani na nje ya nchi.

Sambamba na hayo, Mshote amesema, mahitaji ya mbolea ni makubwa ambapo zinahitajika tani milioni moja ambapo 10% inazalishwa ndani ya nchi na 90% inazalishwa nje ya nchi.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa mbolea Nchini (TFRA) Bw. Joel Laurent amesema, Tanzania ukiweza kuzalisha Mbolea ndani ya nchi, mahitaji ya fedha za kigeni yatakuwa yatapungua kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyo sasa.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli alizipongeza taasisi zilizoshiriki katika hafla hiyo na kuwataka kuhakikisha wanetekekeza kwa vitendo maazimio yote ya kikao hicho.

Pamoja na mambo mengine, hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Madini, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Nishati, GST,  TPDC, NDC, STAMICO, Tume ya Madini na TANESCO.

#vision2030MadininiMaishanaUtajiri#

#UtafitiwaMadiniTanzania