GST yawajengea uwezo watumishi zaidi ya 30 wa ajira mpya.
GST yawajengea uwezo watumishi zaidi ya 30 wa ajira mpya.
Ni katika juhudi za Serikali kuongeza kasi ya utafiti wa madini nchini
Wachimbaji wadogo wa madini wanatarajiwa kunufaika
📍Dodoma, Kongwa
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wake kwa kuwapatia mafunzo kwa vitendo wajiolojia 30 wa ajira mpya, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuongeza kasi ya utafiti wa madini nchini na kuimarisha huduma za kitaalamu kwa wachimbaji wadogo wa madini.
Mafunzo hayo ya Geological Mapping yamefanyika Mei 29, 2026 katika Mlima Mbande, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, yakilenga kuwajengea uwezo wataalamu hao katika ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za jiolojia ambazo ni muhimu katika shughuli za tafiti za madini.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Jiolojia wa GST, Bw. Alex Rutagwelela, alisema kuwa washiriki walipata mafunzo ya vitendo kuhusu namna ya kuchukua taarifa mbalimbali za miamba, ikiwemo ulalo wa miamba (strike, dip na dip direction), pamoja na kutambua na kurekodi mabadiliko ya miamba (alterations) ambayo ni muhimu katika utafutaji wa maeneo yenye madini.
Bw. Rutagwelela alifafanua kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha wataalamu hao kufanya kazi za ukusanyaji wa taarifa za jiolojia kwa ufanisi zaidi katika maeneo mbalimbali nchini, hususan maeneo yenye shughuli za uchimbaji mdogo wa madini.
Aliongeza kuwa kuimarika kwa uwezo wa wataalamu hao kutasaidia kuboresha utengenezaji wa ramani za jiolojia zenye ubora wa hali ya juu, jambo litakalorahisisha utambuzi wa maeneo yenye miamba inayobeba madini ya aina mbalimbali na hivyo kuongeza fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.
Kwa upande wao, wajiolojia waliopata mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na mafunzo ya vitendo waliyoyapata, wakisema yamewaongezea ujuzi na kujiamini zaidi katika kutekeleza majukumu ya utafiti wa madini nchini.
Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa GST kwa kuipatia rasilimali mbalimbali za utekelezaji wa majukumu yake, ikiwemo kuajiri zaidi ya watumishi 50 wa kada mbalimbali hivi karibuni. Hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa taasisi kufanya tafiti za kina za madini, kubaini maeneo mapya yenye rasilimali hizo na kuchochea uwekezaji pamoja na maendeleo ya Sekta ya Madini nchini.

