Watumishi wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini(GST) Washiriki Maadhimisho ya Mei Mosi.
WATUMISHI WA TAASISI YA JIOLOJIA NA UTAFITI WA MADINI TANZANIA (GST) WASHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI.
📍Dodoma
Watumishi wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) wameungana na wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali kushiriki kwa hamasa kubwa katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika Mei 1, 2026 katika Viwanja vya Jamhuri, Mkoani Dodoma.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Mhe.Rosemary Senyamule, amewaongoza mamia ya wafanyakazi waliojitokeza katika kuadhimisha siku hiyo muhimu kwao na kujadiliana Kwa Pamoja namna ya kuboresha utendaji Ili kuwezesha mazingira mazuri ya utendaji Kwa wafanyakazi.
Katika kuonesha mshikamano wao, watumishi wa GST wameshiriki kikamilifu katika maandamano rasmi yaliyoanzia viwanja vya Bunge jijini Dodoma hadi Viwanja vya Jamhuri, sambamba na taasisi nyingine za umma na binafsi, wakionesha umoja, nidhamu na ari ya kuchangia maendeleo ya sekta ya madini na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Ushiriki huo umeakisi dhamira ya watumishi wa sekta ya madini katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kusimamia rasilimali madini kwa tija, pamoja na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo, “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050,” ambayo inalenga kuhamasisha upatikanaji wa ajira zenye staha, kulinda haki za wafanyakazi, na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya muda mrefu.
Kwa ujumla, maadhimisho ya Mei Mosi yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kutambua juhudi na mchango wa wafanyakazi katika kuchangia ukuaji wa uchumi na Maendeleo ya kijamii nchini.

