Wataalamu wa Madini DRC Wajifunza Uzoefu GST
Wataalamu wa Madini DRC Wajifunza Uzoefu GST
📍 Dodoma
Wataalamu wa Madini kutoka Wizara ya Madini ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamefika katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), kwa ajili ya kujifunza shughuli zinazotekelezwa na Taasisi hiyo pamoja na mchango wake katika kukuza na kuendeleza Sekta ya Madini nchini.
Ujumbe huo umepokelewa Agosti 14, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Prof. Abdulkarim Mruma, uliopo katika Ofisi za GST, Dodoma. Ujumbe huo umeongozwa na Bw. Franck Fwamba, Mtaalamu wa Utawala katika Sekta ya Madini na Meneja wa Miradi katika Wizara ya Madini ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Akizungumza katika kikao hicho,Meneja wa Jiolojia wa GST, Bw. Solomon Maswi amesema GST imeendelea kuwa kitovu cha kutoa taarifa sahihi za kijiosayansi zinazotokana na tafiti zinazofanywa na Taasisi, jambo linalowasaidia wadau wa Sekta ya Madini ndani na nje ya nchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu uwekezaji na utekelezaji wa shughuli za madini kwa tija.
Ameeleza kuwa GST inatekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kufanya tafiti za kijiolojia na madini, kutoa taarifa na ushauri wa kitaalamu, kuandaa na kuchapisha machapisho ya kijiosayansi, pamoja na kutoa huduma mbalimbali zinazohusiana na jiolojia na madini.
Aidha, ameeleza kuwa hadi sasa GST imefanikiwa kufikisha upimaji wa kijiolojia katika takribani asilimia 97 ya maeneo ya Tanzania, huku asilimia tatu iliyobaki ikitarajiwa kukamilishwa ifikapo mwaka 2030.
Bw. Maswi pia amefafanua kuwa GST hutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu hali ya jiolojia katika maeneo yanayopangwa kutekelezwa miradi ya ujenzi, hususan majengo makubwa, kwa lengo la kusaidia kuepusha ujenzi katika maeneo yenye changamoto za kijiolojia au mikondo hatarishi chini ya ardhi ambayo inaweza kuathiri uimara wa miundombinu.
Vilevile, amesema GST inashiriki katika kuendeleza utalii wa jiolojia (Geotourism) kwa kutoa utaalamu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo ushiriki wake katika uandaaji wa ramani ya utalii wa jiolojia ya Ngorongoro UNESCO Global Geopark.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maabara wa GST, Bw. Notka Banteze, amesema Taasisi hiyo ina maabara za kisasa zilizo na vifaa vya kisasa pamoja na wataalamu wenye ujuzi na uzoefu mkubwa katika kufanya uchunguzi, upimaji na uchenjuaji wa sampuli mbalimbali za madini.
Ameongeza kuwa maabara za GST zina ithibati ya kimataifa, jambo linalowezesha Taasisi kutoa huduma zenye viwango vinavyotambulika kitaifa na kimataifa. Aidha, amesema GST kwa sasa ina ofisi Dodoma na Geita inayohudumia wateja kutoka Kanda ya Ziwa, huku ujenzi wa ofisi nyingine ukiendelea katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kusogeza huduma karibu zaidi na wadau wa Sekta ya Madini kwa kuzingatia mahitaji ya kila kanda.
Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe kutoka DRC, Bw. Franck Fwamba, amepongeza GST kwa mafanikio iliyoyapata katika tafiti za kijiosayansi na maendeleo ya huduma zake kwa wananchi na Sekta ya Madini kwa ujumla. Bw. Fwamba amesema ujumbe huo umejifunza mambo mbalimbali kupitia uzoefu wa GST, ikiwemo namna Taasisi inavyotekeleza tafiti, inavyotoa huduma za maabara na inavyotumia taarifa za kijiosayansi katika kusaidia maendeleo ya Sekta ya Madini.
Amesema maarifa na uzoefu walioupata kupitia ziara hiyo utakuwa na manufaa katika kuimarisha utekelezaji wa shughuli za Sekta ya Madini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

