Wasira Aitaka GST Kuendeleza Tafiti za Kina katika Sekta ya Madini.
Wasira Aitaka GST Kuendeleza Tafiti za Kina katika Sekta ya Madini.
📍Dar es salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Taifa (Bara) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, ameipongeza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kazi kubwa inayofanya katika utafiti wa madini nchini, huku akiitaka Taasisi hiyo kuendelea kuimarisha tafiti za kina ili kubaini maeneo mapya yenye rasilimali za madini na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Wasira amesema hayo alipotembelea banda la GST katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Akiwa katika banda hilo, alipata fursa ya kujionea huduma mbalimbali zitolewazo na GST na kiwango kilichofikiwa katika kufanya tafiti za madini nchini.
Amepongeza kwa mafanikio yaliyopatikana katika kufanya tafiti za madini nchini, hususan tafiti za jiolojia zilizofanyika kwa asilimia 98, akieleza kuwa hatua hiyo ni msingi muhimu katika kuongeza uwekezaji na kuboresha usimamizi wa rasilimali za madini nchini.
Kwa upande wake, Meneja wa Masoko na Mipango wa GST, Priscus Benard, amesema Taasisi imekuwa ikifanya tafiti za madini nchini kwa ajili ya kuibua maeneo mapya yenye madini ambapo utafiti wa jiolojia umefanyika kwa asilimia 98 , utafiti wa jiofizikia umefanyika kwa asilimia 16 na jiokemia kwa asilimia 24. Tafiti hizi zimefanyika kwa kiwango kidogo kutokana na kutumia gharama kubwa.
Ameshukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kihistoria wa kukubali kutenga asilimia 10 ya makusanyo ya Sekta ya Madini kwa ajili ya kugharamia tafiti za madini nchini.
Amefafanua kuwa kutokana na maamuzi hayo ya Serikali, GST itafanya tafiti za kina kwa kasi zaidi na kwa lengo la kuibua maeneo mapya yenye madini na hivyo kuchochea uwekezaji katika Sekta ya Madini na Sekta nyingine kama ujenzi, viwanda na kilimo.
Aidha, amesema kupitia fedha hizo, GST inalenga kuongeza eneo la nchi lililofanyiwa utafiti wa kina wa jiofizikia kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia asilimia 50; utafiti wa jiokemia kutoa asilimia 24 hadi 62 ifikapo mwaka 2030.

