Matetemeko Sita yatikisa Dodoma, moja Singida ndani ya siku tatu.
Matetemeko Sita yatikisa Dodoma, moja Singida ndani ya siku tatu.
GST: Hakuna madhara yaliyoripotiwa, wananchi watakiwa kuendelea kuchukua tahadhari
Dodoma
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imethibitisha kutokea kwa jumla ya matetemeko saba ya ardhi kati ya tarehe 23 na 25 Juni 2026, ambapo matetemeko sita yalitokea katika Mkoa wa Dodoma na tetemeko moja katika Mkoa wa Singida.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa GST, Mhandisi Ally Samaje, matetemeko hayo yalitokea kati ya saa 6:00 usiku na saa 12:00 asubuhi, yakiwa na ukubwa wa kati ya 2.8 hadi 5.0 katika kipimo cha Richter.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa matetemeko manne yalikuwa na vitovu katika Kijiji cha Haneti, Wilaya ya Chamwino, huku mengine yakitokea katika vijiji vya Mpendo (Chemba), Zamahero (Bahi) na Makuru (Manyoni, Singida).
GST imebainisha kuwa, licha ya matetemeko hayo kusikika katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma, hususan Jiji la Dodoma na maeneo ya jirani, hadi sasa hakuna taarifa zozote za madhara kwa watu au miundombinu zilizopokelewa.
"Hadi sasa GST haijapata taarifa yoyote ya madhara yaliyotokana na matetemeko hayo, isipokuwa yalisababisha taharuki kwa baadhi ya wananchi kutokana na kutokea nyakati za usiku," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
GST imefafanua kuwa matetemeko hayo si jambo la kushangaza kutokana na Tanzania kupitiwa na mikondo miwili ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, ambayo huifanya baadhi ya mikoa ikiwemo Dodoma, Singida, Manyara, Arusha, Mara na Iringa kuwa katika maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kutokea kwa matetemeko ya ardhi.
Aidha, taasisi hiyo imeeleza kuwa maeneo hayo hukumbwa na matetemeko kutokana na mabadiliko ya kijiolojia yanayosababisha miamba iliyopo chini ya ardhi kupata mgandamizo mkubwa na hatimaye kupasuka au kusigana, hali inayosababisha ardhi kutikisika.
GST imekumbusha kuwa hadi sasa duniani hakuna teknolojia inayoweza kutabiri kwa usahihi lini na wapi tetemeko la ardhi litatokea, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kuwa makini na kuzingatia tahadhari zinazotolewa na wataalamu.
Miongoni mwa tahadhari hizo ni kujenga nyumba zinazozingatia viwango vya ujenzi, kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kujenga katika maeneo yenye changamoto za kijiolojia na kuepuka kujenga makazi katika maeneo yenye miamba yenye mipasuko au miinuko hatarishi.
GST imewashauri wananchi kuwa wakati wa tetemeko, waliopo nje ya majengo wabaki katika maeneo ya wazi yaliyo mbali na majengo marefu, miti, nguzo na nyaya za umeme. Kwa waliopo ndani ya nyumba, wanashauriwa kubaki ndani na kujikinga chini ya meza imara, kitanda au kwenye makutano ya kuta yaliyo mbali na madirisha na samani zinazoweza kuanguka.
Baada ya tetemeko, wananchi wametakiwa kuzima umeme katika majengo ili kuzuia hitilafu zinazoweza kusababishwa na mitikisiko inayoweza kuendelea (aftershocks), kukagua usalama wa majengo kabla ya kuendelea kuyatumia na kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo kutatokea madhara yanayohitaji uokoaji.
GST imesisitiza kuwa kuendelea kutoa elimu na kuzingatia tahadhari ni njia muhimu ya kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na majanga ya kiasili, hususan matetemeko ya ardhi

