Mwakilishi toka Ubal...
Mwakilishi toka Ubalozi wa Jamhuri ya Slovakia atembelea Banda la GST, Ajifunza kuhusu Tanzanite na Huduma za taasisi.
03 Aug, 2026
Mwakilishi toka Ubalozi wa Jamhuri ya Slovakia atembelea Banda la GST, Ajifunza kuhusu Tanzanite na Huduma za taasisi.

Mwakilishi toka Ubalozi wa Jamhuri ya Slovakia atembelea Banda la GST, Ajifunza kuhusu Tanzanite na Huduma za Taasisi.

📍Dodoma

Mwakilishi kutoka  Ubalozi wa Jamhuri ya Slovakia, Pavol Popjak, ametembelea banda la Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma, ambapo amejifunza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo katika sekta ya madini.

Akiwa katika banda hilo, Popjak amepata maelezo kuhusu majukumu ya GST katika kufanya utafiti wa jiolojia na madini, utoaji wa huduma za maabara, uchambuzi wa sampuli za madini, pamoja na usimamizi wa taarifa za jiolojia zinazosaidia kukuza uwekezaji na maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Aidha, amefahamishwa kwa kina kuhusu madini ya tanzanite, jiwe la thamani linalopatikana nchini Tanzania pekee, na mchango wake katika uchumi wa taifa kupitia kuongeza thamani ya rasilimali za madini.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Popjak amesema kuwa Slovakia pia ina historia ya uchimbaji wa madini mbalimbali, huku akieleza kuwa wananchi wa nchi hiyo wanajivunia madini ya ganeti nyekundu (Red Garnet), ambayo hutumika kwa kiasi kikubwa katika utengenezaji wa vito vya thamani na pia kama malighafi ya viwandani, hususan katika shughuli za kusaga na kukata kutokana na ugumu wake.

Ameongeza kuwa licha ya uwepo wa uchimbaji wa ganeti nchini Slovakia, uzalishaji wake si mkubwa ukilinganishwa na madini mengine muhimu yanayochimbwa nchini humo, yakiwemo shaba, dhahabu na magnesite.

Ugeni huo umeendelea kuonesha nafasi ya maonesho ya Nane Nane kama jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kuelimisha wadau na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika maendeleo ya sekta ya madini.