Viwanda Vya Uchenjua...
Viwanda Vya Uchenjuaji Madini Geita Huchangia Bilioni 3.2 Kila Mwezi - Waziri Mavunde
15 Nov, 2023
Viwanda Vya Uchenjuaji Madini Geita Huchangia Bilioni 3.2 Kila Mwezi - Waziri Mavunde

Imeelezwa kuwa Viwanda  vya Uchenjuaji Madini mkoani Geita vimeongeza tija katika biashara ya madini nchini ambapo  kiasi cha Shilingi bilioni 3.2  hukusanywa kwa mwezi.
 
Hayo yamebainishwa  Novemba 12, 2023 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akizindua  Ofisi ya kampuni ya  Jema Afrika ambayo inajihusisha na shuguli za  uchenjuaji madini ya  dhahabu mkoani Geita.
 
Mhe.Mavunde amefafanua  kuwa Serikali itaendelea  kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wote katika mnyororo mzima wa sekta ya madini nchini ikiwa pamoja na kuweka mazingira mazuri na salama yenye lengo la kufanya uwekezaji ulio na tija kwa Taifa na jamii kwa ujumla.
 
Akielezea kuhusu  mikakati iliyopo chini ya Serikali ya awamu ya sita, Waziri Mavunde ameleeza kuwa kwasasa kuna mikakati mbalimbali ya mageuzi hususani kwa wachimbaji wadogo kwa kufanya utafiti wa kina utakao toa taarifa sahihi za aina ya miamba na madini iliyopo ili kuchimba bila kubahatisha.
 
Aidha, Waziri Mavunde aliongeza kuwa uchumi wa sasa ni shirikishi hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote ili kufungamanisha sekta zinazotegemeana kiuchumi kama Vision 2030 inavyosema kuwa Madini ni Maisha na Utajiri.
 
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine  Shigela ameipongeza kampuni ya Jema Afrika   kwa kushirikiana na  Serikali katika kutanua wigo wa sekta ya madini  ndani ya mkoa wa Geita.
 
Kwa upande, wake Mkurugenzi Mtedaji wa Jema Afrika Jumanne Bukiri ameishukuru serikali kwa kuweka Sera rafiki kwa wawekezaji ikiwa pamoja kuimarisha miundombinu mbalimbali.
 
Mpaka sasa Mkoa wa Geita una viwanda zaidi 60 vya uchenjuaji madini ya dhahabu katika maeneo ya Nyarugusu , Lwamgasa, Magenge, Kaseme ,Geita na Butobela.
 
VISION 2030: MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI