GST Yaombwa kuongeza...
GST Yaombwa kuongeza elimu kwa wachimbaji wadogo, wahimizwa kuchimba kisayansi
10 Aug, 2026
GST Yaombwa kuongeza elimu kwa wachimbaji wadogo, wahimizwa kuchimba kisayansi

GST YAOMBWA KUONGEZA ELIMU KWA WACHIMBAJI WADOGO, WAHIMIZWA KUCHIMBA KISAYANSI

📍Dodoma

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeshauriwa kuandaa programu maalum za kuwafikia wachimbaji wadogo na kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kufanya utafiti wa kijiosayansi kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji wa madini.

Ushauri huo umetolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ,Mhandisi Aziza Swedi, alipotembelea banda la GST katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Dodoma.

Mhandisi Swedi amesema ni muhimu GST kuwa na mpango endelevu wa kuwafikia wachimbaji wadogo katika maeneo mbalimbali nchini na kuwapatia elimu pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kufanya shughuli za uchimbaji, ili kuwawezesha kuachana na uchimbaji wa kubahatisha.

Amesema elimu hiyo itasaidia wachimbaji wadogo kufanya maamuzi sahihi kabla na wakati wa uchimbaji, ikiwemo kutambua maeneo yenye uwezekano wa kuwa na madini na kutumia taarifa za kisayansi katika shughuli zao.

Aidha, ameitaka GST kuweka utaratibu mzuri wa kufuatilia na kujibu maoni na changamoto zinazowasilishwa na wananchi na wadau wanaotembelea banda la Taasisi hiyo katika maonesho mbalimbali, hususan yale ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi.

“Ni vyema maoni yanayotolewa na wadau katika maonesho yakafuatiliwa na kuwekwa utaratibu wa kuyajibu, hasa yale ambayo hayajapatiwa ufumbuzi, ili wadau waone kuwa maoni yao yanasikilizwa na kufanyiwa kazi,” amesema Mhandisi Swedi.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Swedi ameipongeza GST kwa kasi na juhudi inazofanya katika kutekeleza majukumu yake, akieleza kuwa Taasisi hiyo imekuwa moyo wa Wizara ya Madini kwa kutoa taarifa na takwimu za kitaalamu zinazosaidia Wizara pamoja na Tume ya Madini katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Amesema taarifa zinazotokana na tafiti za kijiosayansi zinazofanywa na GST ni muhimu katika kusaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi na kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini nchini.

Mhandisi Swedi ametoa wito kwa GST kuendelea kuongeza kasi katika tafiti, utoaji wa elimu kwa wadau na ushirikishwaji wa wananchi ili kuhakikisha huduma za Taasisi zinaendelea kuwafikia walengwa katika maeneo mbalimbali nchini.