GST Yahimiza Utalii wa Jiolojia kupitia chemchemu za Majimoto ya Utete, Rufiji
GST YAHIMIZA UTALII WA JIOLOJIA KUPITIA CHEMCHEMU ZA MAJIMOTO YA UTETE, RUFIJI
📍 Rufiji
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Mha. Ally Samaje, amehimiza jamii kuchangamkia fursa za utalii wa jiolojia zinazopatikana katika maeneo yao ili kujipatia kipato na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Mha. Samaje aliyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua shughuli za utafiti wa jiolojia zinazofanyika katika QDS 239, Wilaya ya Rufiji, ambapo GST inafanya utafiti katika eneo la Chemchemi za Majimoto ya Utete.
Katika ziara hiyo aliyoambatana na wataalamu wa jiolojia wa taasisi ,walimweleza Mtendaji Mkuu kwa kina kuhusu asili na mchakato wa kijiolojia unaosababisha kutokea kwa chemchemi hizo, pamoja na namna eneo hilo linavyoweza kuendelezwa na kuwa kivutio cha utalii wa jiolojia.
Wataalamu hao walisisitiza umuhimu wa Chemchemi za Majimoto ya Utete kutambuliwa rasmi kama kivutio cha kijiolojia (Geosite), badala ya kutambuliwa kwa sasa kama kivutio cha ikolojia (Ecological Site) na Halmashauri, ili kuonesha na kutangaza kwa usahihi thamani na upekee wa kivutio hicho. Ushauri huo ulitolewa kwa Afisa Utalii wa eneo hilo, Bw. Laban Emmanuel, kwa lengo la kuweka msingi wa kukitambua na kukiendeleza kivutio hicho kwa mtazamo wa utalii wa jiolojia.
Aidha, GST imeahidi kuhakikisha Chemchemi za Majimoto ya Utete zinaoneshwa kwenye ramani ya jiolojia inayotayarishwa, kwa kuwa eneo hilo lipo ndani ya QDS 239 inayofanyiwa utafiti. Hatua hiyo itasaidia kuongeza mwonekano na utambuzi wa kivutio hicho, pamoja na kutoa taarifa muhimu zitakazochochea utalii na fursa za kiuchumi kwa jamii ya eneo hilo.

