GST, Chuo Kikuu cha Princeton Wagundua Mwamba wa Miaka Bilioni 4.03 Tanzania, Wafungua Fursa Mpya za Utafiti na Geotourism
GST, Chuo Kikuu cha Princeton Wagundua Mwamba wa Miaka Bilioni 4.03 Tanzania, Wafungua Fursa Mpya za Utafiti na Geotourism
📍Dodoma
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Princeton cha nchini Marekani, imefanikiwa kufanya utafiti wa utambuzi wa umri wa miamba mbalimbali nchini na kubaini uwepo wa mwamba wenye umri wa takribani miaka bilioni 4.03, jambo linaloiweka Tanzania miongoni mwa nchi chache duniani zenye miamba ya kale zaidi.
Akizungumza kuhusu matokeo ya utafiti huo, Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Northern Arizona nchini Marekani, Prof. Francisco Apen, amesema uchambuzi wa kisayansi umebaini kuwa mwamba huo ni miongoni mwa miamba ya zamani zaidi kuwahi kutambuliwa duniani, ukiwa na umri unaokadiriwa kufikia miaka bilioni 4.03.
Prof. Apen amesema mwamba huo, unaojulikana kitaalamu kama Fushcite, unapatikana katika eneo la Simba Nguru, mkoani Dodoma, na una sifa za kipekee zinazoutofautisha na miamba mingine yenye umri mkubwa iliyokwisha kugunduliwa katika sehemu mbalimbali duniani.
Kwa upande wake, Meneja wa Ramani na Jiolojia wa GST, Yusto Shine, amesema ugunduzi huo una manufaa makubwa kwa taifa, ikiwemo kukuza utalii wa jiolojia (Geotourism), kuongeza thamani ya urithi wa kijiolojia wa Tanzania pamoja na kuvutia watafiti, wanafunzi na wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi watakaotembelea eneo hilo kwa ajili ya tafiti na mafunzo.
Amesema matokeo hayo yanafungua ukurasa mpya katika tafiti za jiolojia nchini na yanaimarisha nafasi ya Tanzania katika ramani ya dunia ya tafiti za sayansi ya miamba na historia ya awali ya Dunia.
Wataalamu wanaoshiriki utafiti huo wameeleza kuwa baada ya kulinganisha mwamba huo na miamba mingine ya kale duniani, wamebaini kuwa una sifa za kipekee ambazo hazijawahi kuonekana katika miamba mingine yenye umri unaofanana. Kutokana na hali hiyo, timu ya watafiti inaendelea na tafiti za kina katika eneo la Simba Nguru ili kubaini kwa undani zaidi sababu za upekee wa mwamba huo na mchango wake katika kuelewa historia ya awali ya Dunia.

