Waziri Mhe. MAVUNDE...
Waziri Mhe. MAVUNDE Azindua Toleo Jipya la Kitabu cha Madini Viwandani
20 Nov, 2024
Waziri Mhe.  MAVUNDE Azindua Toleo Jipya la Kitabu cha Madini Viwandani

Kitabu chaonesha uwepo wa madini viwanda 43

GST yawakaribisha wadau kutumia taarifa za utafiti.

Dar es salaam

Imeelezwa kwamba Tanzania ina aina mbalimbali za madini ya viwandani ambapo kwa mujibu wa toleo jipya la pili la  kitabu cha madini viwandani kilichoandikwa na  Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kimeonesha aina 43 za madini viwandani ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya viwanda na ufungamanishaji wa sekta za  kiuchumi nchini.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 20,2024 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde  wakati wa uzinduzi wa kitabu cha madini ya viwandani toleo la pili , ikiwa ni siku ya pili Mkutano wa Kimataifa wa uwekezaji Sekta ya Madini 2024.

Waziri Mavunde amesema,  tafiti zinaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi ambapo matarajio ni kuongeza aina nyingine za madini kupitia utafiti wa ndege.

Kuhusu taarifa za tafiti zinazofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Waziri Mavunde ameeleza kwamba , GST ni moyo wa wizara ya madini imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali zinazoibua miradi mikubwa na midogo inayopelekea uanzishwaji wa migodi nchini.

Waziri Mavunde amefafanua kuwa, kitabu cha madini ya viwandani kinaonesha aina za madini 43  yakiwemo madini ya Kinywe,Jasi, Chokaa, Lithium, Helium, Manganese, shaba, chuma, ulanga na mchanga mzito wa baharini pamoja na madini mkakati.

Akielezea umuhimu wa taarifa zinazochapishwa na GST , Waziri Mavunde ameeleza kwamba kupitia taarifa za GST kumekuwepo na miradi mikubwa na midogo iliyoibuliwa na tafiti zilizofanywa na GST.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa GST , Dkt. Mussa  Budeba amewakaribisha wadau wa Sekta ya Madini kutumia taarifa inazochapisha ili kupata uhakika wa taarifa kuhusu mahali halisi madini yanapopatikana nchini.

Dkt.Budeba ameongeza kuwa , sambamba na kitabu cha madini viwandani, GST ina ramani na machapisho mbalimbali yanayoelezea upatikanaji wa madini kupitia utafiti wa jiolojia, jiofiziki na jiokemia.

Kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika Tanzania imekuwa na aina mbalimbali za madini yaliyowekwa kwa mfumo wa makundi yakiwemo , madini ya viwandani , madini ya vito, madini ya metali, madini mkakati , madini adimu (REE), na madini ya nishati.

GST ilianzishwa rasmi mwaka 1925 na Ukoloni wa Mwingireza  wakati huo ikiitwa _British Oversee Management Authority_ yaani (BOMA)