Wachimbaji Madini Nc...
Wachimbaji Madini Nchini Wahimizwa Kufanya Tafiti za Jiosayansi
28 Sep, 2025
Wachimbaji Madini Nchini Wahimizwa Kufanya Tafiti za Jiosayansi

Geita

Wachimbaji wadogo wa madini nchini wamehimizwa kufanya tafiti za jiosayansi  katika  maeneo yao ya shughuli za uchimbaji madini kabla ya kuanza kuchimba ili kujua hali ya jiolojia na uwepo wa madini jambo ambalo litaongeza uzalishaji na kuleta tija ikiwa ni pamoja na kuepusha upotevu wa  mitaji yao. 

Hayo yamesemwa  leo tarehe 28 Septemba, 2025 na Mjiofizikia Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)  Octavian Minja  wakati akiongea na  viongozi wa Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA) waliotembelea banda la GST  katika Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili Manispaa ya Geita. 

Akielezea kuhusu mashine na vifaa vinavyotumiwa na GST  katika tafiti mbalimbali Minja amesema kuwa , GST ina mashine za kisasa ikiwemo mashine ya magnetometer, mashine za GDD (ERT/IP) na ADEM Terramiter  inayotumika katika kubaini sifa za miamba na mbale zinazobabe madini ambazo zinaonesha mwelekeo wa miamba yenye  madini kwa uhakika.

Minja ameongeza kuwa, 
GST ni taasisi ya Serikali yenye dhamana ya kufanya tafiti za madini nchini kwa zaidi ya miaka 100 sasa, kupitia tafiti hizo GST imefanikiwa kukusanya  taarifa nyingi  za jiosayansi katika maeneo mbalimbali ya nchi ambazo ni hazina kwa taifa na wadau wa Sekta ya Madini.

Akielezea kuhusu hali ya  utafiti nchini Minja amefafanua kuwa, mpaka sasa GST imefanya utafiti wa jiofizikia kwa asilimia 16 , jiokemia kwa asilimia 24 na jiolojia kwa asilimia 98 hivyo amewaasa  wachimbaji wa madini nchini hasa wachimbaji wadogo  kutumia taarifa ili kuongeza uzalishaji wa madini na mapato yao kwa ujumla.