Madini, Ufaransa Zaj...
Madini, Ufaransa Zajadili Kushirikiana
19 Feb, 2024
Madini, Ufaransa Zajadili Kushirikiana

Viongozi na Watendaji wa Wizara ya Madini na Taasisi za  Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Tume ya Madini  leo Februari 15, 2023 wamekutana na ugeni wa Kidplomasia kutoka Ubalozi wa Ufaransa nchini na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti ya Ufaransa  (BRGM).

Lengo la ugeni huo  lilikuwa ni  kutambua fursa za uwekezaji hususan  kwenye madini muhimu na mkakati  na  kuangalia maeneo ya ushirikiano  katika Sekta ya Madini nchini.

Katika kikao hicho kilichongozwa na Naibu Katibu Mkuu Msafiri Mbibo, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba  amebainisha maeneo muhimu ya ushirikiano kuwa ni  pamoja  na uwekezaji katika  shughuli za utafiti wa kina wa madini na kuwajengea uwezo wanasayansi katika maeneo mbalimbali ya jiosayansi.

Masuala mengine yaliyogusiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wanajiosayansi kwenye masuala yanayohusu majanga ya asili ikichukuliwa mfano wa tukio la hivi karibuni lililotokea Wilayani Hanang la kumomonyoka kwa udongo na masuala yanayohusu akili bandia.

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Mbibo ameueleza ujumbe huo kuwa bado ipo nafasi ya kukutana na kuendeleza ushirikiano baina yao na GST katika maeneo yaliyokubalika.