GST Yaja na Teknolojia ya Kisasa ya Utafiti wa Madini kwa Bei Nafuu

Wachimbaji Wadogo Waaswa Kuchangamkia Fursa za Utafiti katika Leseni Zao kwa Gharama Nafuu.
📍 Geita
Kwa muda mrefu Wachimbaji Wadogo wamekuwa wakichimba kwa kubahatisha, mara nyingine wakipoteza mitaji yao yote kwa sababu ya kukosa taarifa za uhakika kuhusu maeneo yenye rasilimali. Lakini Serikali sikivu imeleta suluhisho la kudumu.
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeendelea kuleta mageuzi kwenye Sekta ya Madini kupitia huduma za utafiti wa madini kwa teknolojia ya kisasa, zikiwa na gharama nafuu inayowalenga hasa kundi la Wachimbaji Wadogo. Lengo likiwa kuondoa uchimbaji wa kubahatisha na kuhakikisha kila shilingi inayowekezwa inaleta matokeo.
Akizungumza mapema leo Septemba 24, 2025, Mjiofizikia Mkuu wa GST, Octavian Minja amewasisitizia wachimbaji wadogo wanaotembelea banda la GST katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili – Geita, kuwa ni muhimu kufanya tafiti za jiosayansi kabla ya kuanza uchimbaji ili kuongeza uzalishaji na kuepuka hasara.
“Wachimbaji wadogo wanapaswa kuchangamkia fursa hii. Kupitia huduma zetu, wanaweza kupata taarifa za kitaalamu kabla ya kuwekeza mitaji yao. Hii itapunguza hasara na kuongeza tija,” anasisitiza Minja.
Anabainisha kuwa wachimbaji wengi wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na taarifa sahihi za jiosayansi zinazoonesha miamba, madini na mwelekeo wa miamba husika, hali inayowasababisha kuchimba kwa kubahatisha na kupoteza mitaji.
Kwa mujibu wa Minja, GST inatumia vifaa vya kisasa vya jiofizikia vinavyoweza kubainisha aina ya miamba iliyopo chini ya ardhi na mwelekeo wa miamba iliyobeba madini.
“Tunawaalika wachimbaji wote nchini kuitumia GST hususan katika hatua ya utafutaji ili kuepuka kupoteza mitaji na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na uchimbaji holela,” anasisitiza Minja.
Huduma hizi zimeletwa mahsusi kuendana na uwezo wa kifedha wa wachimbaji wadogo, huku zikitoa matokeo sahihi na ya haraka. Tayari wachimbaji waliotembelea banda la GST wameonesha shauku kubwa na nia ya kuitumia GST katika shughuli zao za utafiti wa madini
Kwa maneno mengine, GST imekuwa daraja kati ya teknolojia ya utafiti na mchimbaji mdogo. Matokeo yake ni uchimbaji wa uhakika, mitaji salama, na uchimbaji wenye tija