GST na GTK - Finland...
GST na GTK - Finland Kushirikiana katika tafiti za madini Nchini.
26 Mar, 2024
GST na GTK - Finland Kushirikiana katika tafiti za madini Nchini.

GST NA GTK-FINLAND KUSHIRIKIANA KATIKA TAFITI ZA MADINI NCHINI

GTK kuijengea uwezo GST katika nyanja ya Teknolojia na Utafiti wa Madini

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Taasisi ya Jiolojia ya Finland (GTK) kwa ajili ya kushirikiana kufanya tafiti za miamba na madini pamoja na kubadilishana uzoefu katika teknolojia hususan kwenye shughuli za utafiti.

Utiaji Saini wa Makubaliano hayo umefanyika leo Machi 21, 2024 katika kikao kati ya viongozi wa Wizara ya Madini na Taasisi hizo mbili kilichofanyika kwa njia ya mtandao (Zoom meeting).

Akizunguza katika hafla ya Utiaji saini Makubaliano hayo, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba ameishukuru GTK kwa kukubali kushirikiana na taasisi anayoiongoza katika kufanya tafiti za miamba na madini na kuwajengea uwezo wataalam wa GST kutokana na GTK kuwa na uzoefu wa muda mrefu kwenye shughuli za utafiti wa madini.

Aidha, Dkt. Budeba amesema Tanzania ina taarifa za kina za utafiti wa madini kwa asilimia 16 pekee hivyo mashirikiano hayo yataisaidia Tanzania kuongeza wigo wa maeneo yenye taarifa za utafiti wa kina wa miamba na madini kwa angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Naye, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga amesema makubaliano hayo yametokea wakati muafaka ikiwa Dunia inauhitaji mkubwa wa Madini Mkakati hivyo, tafiti zitakazofanywa na taasisi hizo mbili zitapelekea kubainishwa kwa maeneo mapya yenye hifadhi ya madini hayo.

Akizunguza kwa njia ya mtandao Mkurugenzi Mtendaji wa GTK Prof. Kimmo Tiilikainen amesema Finland ina teknolojia kubwa na uzoefu wa muda mrefu katika Sekta ya Madini hususan kwenye shughuli za utafiti wa madini ambapo ameahidi kwamba wataalam wake watashirikiana na wataalam wa GST kufanya tafiti na kubadilishana uzoefu katika Sekta ya Madini.

Pia, Balozi wa Finland nchini Tanzania Theresa Zitting amesema, GTK ilianzishwa mwaka 1885 ambayo ina uzoefu wa muda mrefu na teknolojia kubwa katika shughuli za utafiti ambapo GST ilianzishwa mwaka 1925 hivyo, kana umuhimu wa kuitumia taasisi hiyo ya nchini Finland kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalam wa GST kwa lengo la kuwaongezea ujuzi hususan katika nyanja ya teknolojia na utafiti wa madini.

Awali, Viongozi na Watumishi wa Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake waliungana kwa pamoja kushuhudia makabidhiano ya Leseni Kubwa ya uchimbaji madini ya Mchanga Mzito wa Baharini kwa Kampuni ya Nyati na Leseni Kubwa ya Usafishaji wa Madini ya Nikeli kwa Kampuni ya Tembo Nikel ambapo hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Dodoma Hotel.

Wizara ya Madini imekuja na Kauli mbiu isemayo "Vision 2030 Madini ni Maisha na Utajiri" ili kuhakikisha nchi ya Tanzania inafanyiwa utafiti wa kina wa jiofizikia kwa kutumia ndege  kwa angalau asilimia  50 ya nchi nzima ambapo kwa sasa utafiti huo umefanyika  kwa asilimia 16 pekee.