Februari 8, 2021, Waziri wa Madini Doto Biteko amekutana na Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) na kuzungumza juu ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo.

Akielezea juu ya mafanikio ya Sekta ya Madini, Waziri Biteko alisema kuwa, Uti wa Mgongo wa Sekta ya Madini ni GST ambao ndio watafiti wa madini nchini.

Waziri Biteko amewataka pia wajumbe wa Bodi ya GST kujifungia ndani na kujadiliana ili kujua kitu gani wafanye kitakacho ifanya GST ijiendeshe yenyewe.

Aidha, Waziri Biteko aliongeza kuwa, anatamani kuona mabadiliko ya Sekta ya Madini nchini yanaenda sambamba na ukuaji wa Taasisi ya GST.

“Kiu yangu ni kuona GST inakua na inajiendesha yenyewe ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato zaidi tofauti na ilivyo sasa,” amesema Waziri Biteko.

Pia, Waziri Biteko amesema, GST inatakiwa ijitangaze ndani na nje ya nchi ambapo ameitaka bodi hiyo kushiriki kikamilifu katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta Madini utakaoanza Februari 21 mpaka 24 ili kutumia fursa hiyo kujitangaza nje na ndani ya nchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila ameipongeza GST kwa kushiriki katika kazi za kisekta akitolea mfano GST ilivyoongoza timu ya uchunguzi wa upatikana madini ya Urenium wilayani mvomero mkoani Morogoro ambapo mpaka sasa matokeo ya tafiti huo yapo katika hatua za mwisho.

Awali, akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya GST Prof. Justinian Ikingula alianza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuiwezesha GST kutimiza majukumu yake.

Akifafanua juu ya uwezeshaji huo Prof. Ikingula alisema kuwa serikali imeipatia GST kiasi cha Tshs. Bilioni 3.3 ambazo zimewezesha GST kununua vifaa mbalimbali vya maabara ikiwa na pamoja na ununuzi wa magari sita ambayo yatarahisisha utendaji kazi wa taasisi hiyo.

Akisoma taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya GST, Prof. Ikingula alieleza Kuwa GST imeshiriki katika tafiti mbalimbali za jiosayansi kama vile utafiti wa jiosayansi katika mji wa serikali (Mtumba),Mradi wa Ujenzi wa reli ya mwendokasi pamoja na mradi wa Bwawa la uzalishaji umeme lijulikanalo kwa jina (Mwalimu Nyerere Hydro Power).

Mkutano huu ni utaratibu wa waziri wa kukutana na bodi za taasisi zilizochini ya wizara ya madini.

Zifuatazo ni picha mbalimbali za mkutano huo