• GST isaidie kuwapatia maeneo wachimbaji wadogo yenye Taarifa za Utafiti wa Jiolojia

• GST iongezewe uwezo kwa ajili ya kufanya utafiti zaidi wa kina.

• GST ni muhimu sana Katika sekta ya Madini na wadau wengi wanahitaji

Samwel Mtuwa na Tito Mselem – DODOMA.

Utafiti wa Madini nchini ndiyo moyo wa maendeleo ya Sekta ya Madini utakao ifanya sekta hiyo isonge mbele na kuongeza tija katika uendeshaji wake ikiwa pamoja na kugundua maeneo mapya ya uwekezaji.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko wakati akizindua Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) iliyozinduliwa rasmi leo Septemba 22, 2022 katika ukumbi wa Abdukarim Mruma uliopo jijini Dodoma.

Dkt. Biteko amesema kuwa ili kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa (GDP), GST kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lazima ziongeze wigo wa kufanya tafiti kwa lengo la kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapa maeneo yenye taarifa za uwepo wa mashapo katika maeneo yao ya uchimbaji madini.

Natamani kuona Sekta ya Madini ikiendelea kuchangia fedha za kigeni kwa kiasi kikubwa hivyo niwatake GST, Tume ya Madini na STAMICO kutengeneza utaratibu wa kukutana mara kwa mara ili mpange namna bora ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wa Madini wanaofanya uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali amesema Dkt. Biteko.

Akizungumzia kuhusu ushirikiano na uzoefu wa kikazi, Dkt. Biteko ameeleza kwamba uzoefu ukitumika vizuri unaweza kujenga mafanikio ya muda mrefu tena kwa uhakika lakini hasara za uzoefu ni kufunga milango ya kujifunza zaidi ambapo amesema uzoefu walionao Wajumbe wa Bodi ya GST usiwafanye kuacha kujifunza zaidi.

Aidha, Dkt. Biteko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo na miongozo anayoitoa ili kuisimamia vyema sekta ya Madini ikiwa pamoja na kumteua tena Mwenyekiti wa Bodi ya GST Profesa Justinian Ikingula.

Pia, Dkt. Biteko ameitaka GST kushirikiana na Sekta binafsi kufanya tafiti ili kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini nchini kwa lengo la kuongeza tija na kuepuka uchimbaji wa kubahatisha hii ni kutokana na Utafiti wa madini utumia gharama kubwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema GST ni taasisi muhimu katika ukuaji wa Sekta ya Madini hivyo ameitaka Wizara iiongezee uwezo taasisi hiyo ili iweze kufanya tafiti za kutosha.

Nae Mtendaji Mkuu wa GST Dkt.Mussa Budeba amemshukuru Waziri wa Madini Dkt. Biteko kwa ushirikiano anaoupata kutoka katika Uongozi wa Wizara ya Madini ambao unaleta matokeo chanya Katika utendaji na utekelezaji wa majukumu ya GST.

Mapema kabla ya kufunga uzinduzi huo mwenyekiti wa Bodi ya GST Profesa Justinian Ikingula alimshukuru Waziri wa Madini Kwa kukubali kuzinduzia Bodi mpya ya GST na kutoa picha ya mwelekeo wa Bodi utakaoiwezesha GST kufanikisha malengo iliyojiwekea chini ya usimamizi wa Bodi.

Awali, Dkt. Biteko alikutana na ujumbe kutoka Japan uliobebwa na Balozi wa Japan nchini Tanzania Yasushi Misawa ambapo wakijadiliana kuhusu fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini zilizopo nchini Tanzania.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Biteko amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali yakiwemo madini ya kimkakati kama vile Nikeli, Kinywe na mengine mengi hivyo ameimba nchi ya Japan kupitia Balozi wake kuwekeza katika sekta hiyo nchini Tanzania.