Tarehe 12/8/2020 majira ya saa 2:13 usiku kulitokea tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 5.9 katika kipimo cha Richter ambalo kitovu chake kilikuwa ndani ya Bahari ya Hindi katika Latitude 7.37 (Kusini) na Longitudo 39.91 (Mashariki) umbali wa takriban kilomita 90 Kusini Mashariki ya Jiji la Dar es Salaam.
Tetemeko hilo lilitokana na nguvu za asili za mgandamizo kwenye matabaka ya miamba chini ya bahari. Aidha, eneo hilo lipo kwenye mkondo wa mpasuko wa miamba (Davie’s Ridge) ambao huanzia magharibi ya Kisiwa cha Madagasca na kupita katika Pwani ya Tanzania ambapo kumekuwa na matukio ya matetemeko ya ardhi hususan katika Pwani ya Mtwara kama inavyoonekana katika ramani hapo chini.
Tetemeko hilo lilisikika katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Tanga, Arusha na Kilimanjaro. Hatahivyo, hadi hivi sasa GST haijapokea taarifa zozote za kutokea kwa madhara kutokana na tetemeko hilo. Juhudi zinaendelea kufanyika ili kupata taarifa endapo kuna madhara yametokea.

Ramani inaonesha vitovu vya matetemeko ya ardhi yaliyowahi kutokea nchini na tetemeko la tarehe 12/8/2020 (mduara mwekundu).


Imetolewa na:
TAASISI YA JIOLOJIA NA UTAFITI WA MADINI TANZANIA (GST)