Tarehe 24/8/2020 majira ya saa 4:03 asubuhi kulitokea tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 5.0 katika kipimo cha Richter ambalo kitovu chake kilikuwa ndani ya Ziwa Nyasa katika Latitude 11.27 (Kusini) na Longitudo 34.6 (Mashariki) umbali wa takriban kilomita 126 Kusini-Magharibi ya Mji wa Songea, na kilomita 24 Kaskazini-Magharibi ya Mji wa Mbamba Bay, kilomita 15 Kusini-Magharibi ya Mji wa Liuli na kilomita 51.9 Kusini-Magharibi ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma.
Tetemeko hilo lilitokana na nguvu za asili za mgandamizo kwenye matabaka ya miamba ndani ya Ziwa Nyasa. Tetemeko hilo lilisikika katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Ruvuma na nchini Malawi. Hatahivyo, hadi hivi sasa GST haijapokea taarifa zozote za kutokea kwa madhara kutokana na tetemeko hilo. Juhudi zinaendelea kufanyika ili kufuatilia na kupata taarifa endapo kuna madhara yaliyosababishwa na tetemeko hilo.

Ramani inaonesha vitovu vya matetemeko ya ardhi yaliyowahi kutokea nchini na tetemeko la tarehe 24/8/2020 (mduara mwekundu) ndani ya Ziwa Nyasa

Imetolewa na:
TAASISI YA JIOLOJIA NA UTAFITI WA MADINI TANZANIA (GST)
25/8/2020