UTANGULIZI

Mnamo tarehe 17/12/2019 GST ilipokea taarifa ya kutokea kwa tukio ambalo lilisadikiwa kuwa ni volkano katika kijiji cha Tatwe Mkoani Mara. Taarifa kuhusiana na tukio hilo zilitangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini na kupitia mitandao ya kijamii zikielezea tukio hilo ambalo lilisababisha sinto fahamu kwa wakazi wa kijiji cha Tatwe na vitongoji vyake.
Milipuko ya volkano ni mojawapo ya majanga ya asili ya jiolojia, ambapo moja kati ya majukumu ya GST ni uratibu wa majanga ya asili ya jiolojia. Kwa kuzingatia hilo GST mnamo tarehe 18/12/2019 ilituma wataalamu kufika katika eneo la tukio ili kufanya uchunguzi kubaini chanzo na kuufahamisha umma kuhusu tukio hilo. Wataalamu kutoka GST ni Dr. Mussa Budeba ambaye ni Mtendaji Mkuu, Bw. Gabriel Mbogoni ambaye ni Mjiolojia Mwandamizi na Bi. Christina Andrea ambaye ni Fundi Sanifu Jiolojia. Wataalamu hao waliambatana na Maafisa wafuatao kwa niaba ya uongozi wa Wilaya:- Bw. Nyaisara Mgaya ambaye ni Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mara, Bi. Diana Constantine ambaye ni Afisa Majanga ya asili wa Wilaya ya Rorya, Bw. Mussa Indason Seda ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Tatwe. Wengine ni Bw. Julius Odera Ochiwachi ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Tatwe, Bw. Kelvin Chacha Odwee ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sang’ombe pamoja na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Tatwe.

MBINU ZA UCHUNGUZI “Methodology
Mbinu zilizotumika katika kufanya uchunguzi ni pamoja na kusoma ramani na taarifa za jiolojia zilizochapishwa kutokana na tafiti za jiolojia za hapo awali (QDS 4 & 5 –North Mara, Tarime), kuchunguza aina ya miamba na matabaka ya udongo katika eneo husika na kukusanya sampuli za maji kwa ajili ya uchunguzi katika maabara kubaini viasili vya madini vilivyomo katika sampuli hizo.

MATOKEO YA UCHUNGUZI
Baada ya kufanya uchunguzi katika eneo la tukio ikiwa ni pamoja na kufanya mahojiano na wananchi wa eneo husika ambao inasemekana kwamba walishuhudia tukio hilo, wataalamu walibaini kwamba tukio hilo lilikuwa limetafasiriwa vibaya huenda kwa sababu ya kukosekana kwa maelezo ya kitaalamu hali iliyowafanya wakazi hao kuwa na maoni tofauti kuhusiana na tukio hilo. Taarifa zilizotolewa na baadhi ya mashuhuda hao (Bibi. Rosemary Joshua Ayodo na Bw. Samson Joshua Ayodo) zilieleza kwamba siku ya tukio kulinyesha mvua kubwa sana iliyoambatana na upepo mkali, na vumbi jingi ambalo lilidhaniwa ni moshi wa volkano na kwamba wakati mvua hiyo ikiendelea kulisikika kishindo kikubwa ambacho kilidhaniwa ni tetemeko la ardhi.
Tafasiri sahihi ya kitaalamu ya tukio hilo ni kwamba yalikuwa ni maporomoko ya ardhi (landslide). Uchunguzi ulibaini kwamba eneo hilo lipo katika bonde (valley) ambalo ni makutano ya vilima vya Tatwe (Tatwe Hill) na Nyalgego (Nyalgego Hill) ambapo maji hutiririka kupitia bonde hilo hadi Mto Chirya. Kutiririka kwa maji hayo hususan wakati wa msimu wa mvua (surface run-off) husababisha mmomonyoko ambao humeng’enya miamba na udongo katika maeneo ya miinuko na kujikusanya kwenye bonde hilo (sedimentation). Kwahivyo eneo la bonde hilo lilikuwa na matabaka ya udongo na miamba ambayo hayajajishindilia (unconsolidated sediments).
Ikumbukwe kwamba tabaka la udongo huundwa na chembechembe za udongo ambazo katikati yake huwa kuna sehemu za wazi (pore space) ambazo huhifadhi maji. Chembechembe za udongo na maji yaliyomo kwenye sehemu za wazi katika udongo huwa katika hali ya uwiana (equilibrium). Lakini pindi kiasi cha maji kinapokuwa kingi kuzidi kiasi ambacho udongo huo unaweza kuhifadhi (liquid limit), na kutokana na msukumo wa maji yaliyomo katikati ya chembechembe za udongo (pore pressure) husababisha tabaka hilo la udongo kuvurugika na hatimaye kuwa tope na hivyo kuwa rahisi kuporomoka kuelekea bondeni. Endapo kutakuwa na majabali ya miamba kama ilivyokuwa kwenye eneo hilo la Tatwe majabali hayo huongeza uzito na hivyo kuwa rahisi matabaka hayo ya miamba na tope kuporomoka kwa kasi na kusababisha kishindo.

HITIMISHO NA USHAURI
GST inapenda kuutarifu umma wa Watanzania kwamba tukio la tarehe 11/12/2019 lililotokea katika Kitongoji cha Sang’ombe katika Kijiji cha Tatwe, Kata ya Gulibe Wilayani Rorya Mkoa wa Mara lilikuwa ni MAPOROMOKO YA ARDHI na kwamba SIYO VOLKANO. Taarifa zaidi ya kina kuhusiana na tukio hilo itatolewa katika taarifa ya Hitimisho baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa sampuli zillizokusanywa kutoka kwenye eneo hilo. GST inapenda kuwashauri wananchi kuchukua tahadhari hususan wale wanaoishi kwenye maeneo ya miinuko ambayo ianaambatana na majabali makubwa ya mawe kwavile mabadiliko ya jiolojia katika miamba hutokea kila siku ambapo miamba huendelea kudhoofu siku hadi siku. Wanashauriwa kuachana na kasumba ya kuamini kwamba hapajawahi kutokea matukio ya kuporomoka kwa mawe katika maeneo yao katika kipindi kirefu cha umri wao, kwavile matukio ya kudhoofu kwa miamba huchukua miaka mingi kitendo ambacho ni vigumu kukishuhudia, hivyo muda wote wanapaswa kuwa katika hali ya tahadhari. Ikumbukwe kwamba matetemeko ya ardhi ambayo ni matukio yasiyotabirika, yanaweza kusababisha kuporomoka kwa majabali ya miamba katika maeneo ya miinuko, hivyo wanapaswa pia kuchukua tahadhari muda wote. GST inapenda kuwaasa wananchi kutoa taarifa za matukio yasiyo ya kawaida katika maeneo yao kupitia kwa uongozi ili taarifa hizo ziweze kuzifikia mamlaka husika kwa wakati na hivyo kuwezesha wahusika ama wataalamu kufika kwenye eneo la tukio kwa wakati.

Imetolewa na:
TAASISI YA JIOLOJIA NA UTAFITI WA MADINI TANZANIA (GST)
19/12/2019