Tarehe 28 Februari, 2023, Bw. Mouhamad Altesbehji ambaye ni mwekezaji kutoka Dubai chini ya kampuni ya GOLDOROX TANZ LTD amesema amevutiwa na kasi na weledi uliooneshwa na wataalam wa GST wanaoendelea kufanya utafiti wa madini katika leseni zake zilizopo Wilaya ya Chunya.
“Nimeridhishwa sana na utendaji kazi wa GST, wataalamu wameonesha uzoefu na weledi mkubwa sana…mna vifaa vya kisasa…. GST mpo vizuri”. Aliongeza mwekezaji huyo.
Aidha, mwekezaji huyo alisema kuwa kwa kasi ambayo wataalamu wa GST wameonesha katika kufanya utafiti huo, anaamini kazi hiyo itakamilishwa kwa wakati. Pia, ameipongeza GST kwa namna ilivyoratibu utekelezaji wa kazi yake.

Awali akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya kazi hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Jiolojia wa GST, Dkt. Ronald Massawe alisema kuwa kazi inaendelea vizuri kama ilivyopangwa na mteja atapatiwa ripoti yake kwa wakati ili imsaidie kufanya maamuzi sahihi kwenye utafiti wa kina ukiwemo uchorongaji. Akielezea utekelezaji wa utafiti huo, Dkt. Massawe alisema GST imejipanga vizuri na kazi hiyo ya utafiti inafanywa na timu tatu za wataalamu ambazo ni timu ya jiolojia, jiokemia na jiofizikia. Kila timu inaendelea na kazi yake kama ilivyojipangia.

Naye mtaalam wa GST alieambatana na timu hii wakati wa ukaguzi wa namna kazi inavyofanyika Mjiolojia Mwandamizi Charles Moye ameelezea namna utafiti ulivyofanyika na hatua uliofikia sambamba na jiolojia inavyojipambanua kwenye eneo la utafiti.

Katika ziara hiyo ya kukagua maendeleo ya kazi hiyo Dr. Massawe aliambatana na Kaimu Meneja sehemu ya Jiolojia Bw. Maswi Solomon, Meneja Masoko na Mipango Bw. Priscus Benard na Mkaguzi Mkuu wa Ndani CPA Timoth Mbulla. Lengo kuu likiwa ni kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa kazi hiyo kwa mujibu wa viwango vya ubora vilivowekwa.

Zifuatazo ni picha mbalimbali za matukio