Ziara ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Serikali Awamu ya Sita kwa kuipatia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) vifaa na mashine za kisasa kwa ajili kuongeza wigo wa utafiti wa madini nchini.

Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 14 Machi 2023 na makamu mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Judith Kapinga mbunge wa viti maalum wakati akiongea na vyombo vya habari mapema baada ya kukamilisha ziara hiyo.

Ziara hiyo ya kutembelea maabara za GST kwa ajili ya kujionea utekelezaji wa majukumu ya GST, Mhe. mbunge Judith Kapinga aliipongeza serikali kwa kuwekeza mashine za kisasa katika kufanya uchunguzi, utambuzi na unjenjuaji wa madini mbalimbali.
“kwa kweli niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi inazofanya katika kuiwekeza taasisi yetu ya GST kwa kuipatia mashine mbalimbali za uchunguzi , utambuzi na uchenjuaji wa madini” alisema kapinga

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Songwe Philipo Mulugo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati hiyo alishauri kuwa katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2023/2024 GST iongezewe nguvu zaidi ya kibajeti ili kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Kabla ya ziara hiyo kuanza, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba aliwakaribisha wajumbe wa Kamati na kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa wanaotoa katika kusimamia GST katika kutekeleza majukumu yake.

“Ninashukuru sana Kamati hii kwa usimamizi wake nzuri ambao umeendelea kuifanya GST kuboreka zaidi katika utoaji wa huduma zake.” Alisema Dkt. Budeba.

Mapema baada ya utambulisho huo Dkt. Budeba alimkaribisha Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa kwa ajili ya kuanza ziara hiyo ambapo Dkt. Kiruswa aliishukuru Kamati kwa namna mnavyoendelea kuishauri na kuisimamia Wizara ya Madini kwa ufanisi mkubwa.
“Sisi tunafarijika sana kwa namna mnavyotusimamia Wizara na Taasisi zake na tunawakaribisha GST muweze kujionea mlichokisoma kwenye taarifa zetu”. Aliongeza Dkt. Kiruswa

Katika ziara hiyo wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali juu ya utekelezaji wa majukumu ya GST hasa juu ya uchunguzi wa sampuli za madini katika maabara ya GST.