Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Dastan L. Kitandula;
Naibu Waziri wa Madini, Mheshimiwa Stanslaus Nyongo;
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini;
Katibu Mkuu, Prof. Simon Samwel Msanjila;
Mwenyekiti wa Bodi, Prof.Justinian Ikingura;
Wajumbe wa Bodi;
Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST; Yokberth Myumbilwa;
Wakuu wa Idara mliopo;
Wageni waalikwa;
Watumishi wa GST;
Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana;
Habari za Asubuhi;
Awali ya yote ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema kwa kutujaalia uzima, nguvu na afya njema na kutuwezesha kukutana hapa leo katika siku hii muhimu.
Aidha, napenda nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa heshima kubwa mliyonipa ya kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika hafla hii ya Uzinduzi wa Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).
Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi
Napenda pia nitumie fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwako wewe Mwenyekiti pamoja na wajumbe wote wa Bodi ya GST kwa kuteuliwa kwenu kuwa wasimamizi wa utekelezaji wa kazi za taasisi hii.
Kuundwa kwa Bodi
Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi
Mtakumbuka kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt John Joseph Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanya Marekebisho katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa Serikali katika Sekta ya Madini ili rasilimali madini tulizojaliwa na Mwenyezi Mungu ziwanufaishe watanzania wote. Kwa mujibu wa Marekebisho hayo ya Sheria sambamba na Kanuni zake za Mwaka 2018, (GN.6 Sehemu ya 2 kifungu 3-1), Bodi ya GST imeundwa ili kusimamia utekelezaji wa majukumu ya GST. Kanuni hizo zimeainisha kuwa Bodi ya GST itaundwa na:-
- Mwenyekiti ambaye atateuliwa na Rais
- Katibu wa Kamisheni ya Madini
- Kamishna wa Madini
- Mwanasheria kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
- Wataalamu watatu (3) wenye uelewa na uzoefu mkubwa kwenye masuala ya madini ambao watateuliwa na Waziri wa Madini
Aidha, Mtendaji Mkuu wa GST atakuwa Katibu wa Bodi hii.
Naomba kutoa tamko kwenu kuwa uteuzi wa Mheshimiwa Rais kwa Mwenyekiti na uteuzi wa Waziri kwa wajumbe wa Bodi umefanyika kwa mujibu wa Sheria na umezingatia vigezo vingi ikiwemo uadilifu na uzalendo wenu kwa nchi yetu. Ni matarajio yangu kuwa mtafanya kazi yenu kwa uadilifu na uweledi wa hali ya juu kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
Muda wa Bodi
Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi
Bodi ya GST itafanya kazi zake kwa kipindi cha miaka mitatu. Naomba ieleweke kwamba mjumbe yeyote baada ya kipindi cha miaka mitatu kumalizika anayo fursa ya kuteuliwa tena kufanya kazi na GST endapo Mheshimiwa Rais na Waziri wa Madini wataona inafaa kufanya hivyo kwa manufaa ya taasisi na taifa kwa ujumla.
Mamlaka na Majukumu ya Bodi
Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi
Mtapatiwa makabrasha ambayo ndani yake kuna maelezo kwa kina kuhusiana na majukumu ya GST na ni imani yangu kuwa mtakapoyasoma mtapata uelewa juu ya majukumu ya taasisi hii. Mimi nitajielekeza kwenye majukumu ya Bodi. Kanuni za Madini (Mining Regulations) za Mwaka 2018 zinaainisha wazi majukumu ya Bodi hii, naomba nitaje machache ambayo ni kutathmini (asses) utendaji kazi wa GST; kupitisha bajeti ya taasisi; kusimamia utekelezaji wa majukumu ya GST na kuhakikisha GST inajengewa uwezo ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi
Pamoja na majukumu ya Bodi ambayo nimeyataja, ninaomba nisisitize utekelezaji wa jukumu lililotokana na Marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kupitia the Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, Na. 7 ya mwaka 2017 Kifungu 27F (1), (2), (3). Kifungu hiki kinaitaka GST kukusanya, kuhakiki, kutafasiri na kuhifadhi kumbukumbu zote za kanzidata zitokanazo na utafiti pamoja na uchimbaji wa madini kwa lengo la kubainisha uhalisia wake. Ninawasihi, sote tuunge mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano zinazoitaka Taasisi kutekeleza jukumu hilo.
Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi
Ninatambua miongoni mwenu kuna Kamishna wa Madini, Kamishna wa Tume ya Madini na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ambako leseni zote za utafiti na uchimbaji wa madini zinatolewa, hivyo ni matumaini yangu kuwa mtatoa ushirikiano mkubwa kwa GST kwa kiasi kikubwa namna ya kupata taarifa hizo hata zile ambazo utafiti ulishaisha. Nitafurahi kuona kuwa Bodi hii inaweka mikakati thabiti ya kupata taarifa hizo. Taarifa hizo ni muhimu sana kwa nchi na kwa uwekezaji katika sekta hii ya madini hasa kwa wachimbaji wadogo ambao hawana uelewa mpana wa jiolojia.
Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi
Naomba nikutanabahisheni kwa mara nyingine tena kwamba kazi mliyokabidhiwa na Serikali ni kubwa na nyeti sana kwa maendeleo ya Sekta ya Madini. Hivyo nina matumaini makubwa kwamba, mtatekeleza majukumu hayo na mengine ambayo sikuyataja lakini yameelezwa katika Sheria na Kanuni husika ili kuhakikisha kwamba GST inakidhi matarajio ya wadau na kuleta tija katika utekelezaji wa majukumu yake kwa maendeleo ya Sekta na Taifa kwa ujumla.
Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi
Taasisi mnayosimamia ni Sehemu ya Wizara ya Madini, hivyo nitumie nafasi hii kuwakaribisha sana kwenye familia ya Wizara ya Madini. Ni matarajio yangu mtatekeleza majukumu yenu kwa ushirikiano wa karibu na menejimenti ya GST na Wizara kwa ujumla kwa kuzingatia Sera, Sheria na Kanuni za Wizara.
Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi
Kwa kumalizia napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kukubali uteuzi huu na ninawashukuru wote mlioshiriki kwa namna moja ama nyingine katika uzinduzi huu. Baada ya kusema hayo machache, ninayo heshima kubwa kutamka kwamba, BODI YA GST IMEZINDULIWA RASMI.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA