Na.Samwel Mtuwa – GST.

Leo tarehe 24 Januari, 2022 Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) imeingia makubaliano ya kushirikiana katika kutekeleza majukumu ya taasisi zao.

Kupitia makubaliano hayo GST na UDSM watashirikiana katika kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo utafiti wa madini, uandaaji wa machapisho ya jiosayansi; utoaji wa mafunzo kwa watumishi na uratibu wa majanga asili ya jiolojia yakiwemo matetemeko ya ardhi, maporomoko ya udongo na milipuko ya volkeno.

Awali akizungumza juu ya makubaliano hayo, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Daniel Budeba alisema ushirikiano huu utaongeza ubora wa kazi wa taasisi zote mbili na hivyo kufikia malengo husika.

Dkt. Budeba alifafanua kuwa lengo la Wizara ya Madini ni kuona mchango wake katika pato la Taifa unafikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Ili kufikia lengo hilo, Taasisi ya GST inajukumu la kufanya tafiti za madini ambazo zitazalisha taarifa za jiosayansi zitakazochochea uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini.

Nina Imani kuwa Ushirikiano baina ya GST na UDSM utaongeza ubora wa tafiti zetu na taarifa zake kwa ujumla na hivyo kuchagiza ukuaji wa Sekta ya Madini.

Dkt. Budeba aliongeza kuwa
GST kwa upande mmoja ina uzoefu mkubwa katika tafiti za madini na ndiye taasisi yenye dhamana na masuala ya jiolojia ya nchi, kwa upande wa pili UDSM nayo inauzoefu mkubwa katika ufundishaji, uandaaji wa machapisho mbalimbali ya kitaalamu na katika ufanyaji wa tafiti mbalimbali, hivyo tukiunganisha uzoefu na nguvu za taasisi hizi tunaamini ubora wa kazi zetu utaongezeka zaidi.

Kwa upande wake Dkt. Elisante Mshiu ambaye alimuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema mbali na kunufaika na uzoefu uliopo ndani ya taasisi zote mbili, uwepo wa ushirikiano huu pia utatoa fursa kwa taasisi zote katika kutumia miundominu na vitendea kazi vinavyopatikana ndani ya taasisi hizo.

GST kupitia Wizara ya Madini imeboresha sana vitendea kazi vyake, mashine nyingi za kisasa za kufanya tafiti na uchunguzi wa madini zimenunuliwa.

kupitia ushirikiano huu UDSM itanufaika kwa kutumia mashine hizo na hivyo kuongeza ufanisi zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha, Dkt. Mshiu aliushukuru uongozi wa GST kwa kukubali kuingia makubaliano hayo ambayo yanaenda kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi zote na hivyo kuleta ustawi wa Sekta ya Madini na Taifa kwa ujumla.

Zifuatazo ni baadhi ya picha za tukio Zima la utiani Saini

Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba upande wa kulia na Dkt . Elisante Mshiu kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es salaam (UDSM) wakionesha hati za makubaliano ,kwa wajumbe wa Menejimenti hawapo pichani
Mtendaji Mkuu wa GST Dkt.Mussa Budeba akiongea na vyombo vya habari juu ya makubaliano ya ushirikiano wa kikazi baina ya GST na UDSM , pembeni wanaofuatilia mazungumzo hayo ni wawakilishi kutoka UDSM