Wachimbaji wadogo wa Madini ya Bati wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera wanufaika na ziara ya kikazi ya GST katika maeneo yao ya kazi. Wakizungumza katika mkutano huo, wachimbaji walielezea kero mbalimbali ikiwa pamoja na changamoto ya upimaji wa sampuli za Madini ya bati ili kujua kiwango cha asilimia ya Madini bati yaliyopo kwenye sampuli zao.
Utambuzi huo wa asilimia unawasaidia wao kufanya biashara makini kwa sababu kwa sasa uuza Madini hayo kwa wanunuzi (Dealers) bila kufanya vipimo vyovyote jambo wanalioona ni kama wanamnufaisha mnunuzi. Aidha, bei ya Madini bati kwa kilo inaanzia shilingi elfu thelasini (30,000/=) mpaka elfu arobaini (40,000/=) kutegemea na asilimia ya Madini bati iliyopo kwenye mbale husika.
Kutokana na Hali hiyo wachimbaji wadogo wameiiomba GST kuwasaidia vipimo katika eneo lao ili kuwawezesha kufanya biashara yenye haki na usawa kwa pande zote mbili.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Ofisi ya GST mkoani GEITA Mjiolojia Mwandamizi John Kalimenze aliwaeleza wachimbaji wadogo kuwa Serikali ina dhamira ya dhati kabisa ya kuwasaidia wachimbaji wadogo na kuwahakikishia huduma hiyo imepokelewa na itafanyiwa kazi na GST. Katika mkutano huo, GST kupitia wataalam wake walitoa Mafunzo juu ya njia mbalimbali za utafiti wa Madini ya bati kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi wachimbaji kuendelea kugundua maeneo mengine yenye uzalishaji.
Kulingana na tafiti za GST zilizofanywa mwaka 2014 zilionesha uwepo wa madini bati katika maeneo ya Kaborishoke, Nyabikokolo, Rwariko, Kyerwa Syndicate na Kyabitembe. Maeneo mengine yalionesha viashirio vya madini bati ni pamoja na maeneo ya Kaitambuzi, Mwemage, Murunyinya na Kyabitembe Mashariki na Magharibi.
