Wizara ya Madini chini ya taasisi yake ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), imepokea taarifa ya utafiti wa mfano yaani ( Pilot Project) wa Jiosayansi uliofanyika katika mipaka ya nchi tatu ambazo ni Tanzania , Msumbiji na Zambia , chini ya ushirikiano wa serikali ya Jamhuri ya Korea ya kusini kupitia taasisi ya Jiosayansi na Rasilimali Madini nchini Korea (KIGAM), GeoGeny , NGII za nchini Korea .

Mradi huu umekuwa na manufaa mbalimbali kama vile kuonesha baadhi ya maeneo ya mkoa wa Ruvuma kuonesha uwepo wa miamba yenye madini kama vile chuma na shaba kwenye tabaka la juu la ardhi.

Taarifa zilizochukuliwa na ndege zinaonesha kua kuna baadhi ya maeneo ya mkoa wa Ruvuma yana miamba yenye usumaku mkubwa ambayo inaweza kuashiria uwepo wa madini ya chuma na madini mengine yanayoweza kuambatana na chuma kama vile madini ya metali mafno (Cu. Ni).

Sambamba na maeneo hayo , maeneo mengine yaliyoonekana katika picha zilizochukuliwa na ndege zinaonesha uwepo wa miamba isiyo ambatana na usumaku kama miamba tabaka yaani aidha yenye usumaku mdogo au isiyokuwa na usumaku ambayo yanaashiria uwepo wa madini yasiyokuwa na usumaku kama vile makaa ya mawe na urani.

Pia taarifa kutoka katika picha ya ndege zimeonyesha mipasuko (lineaments) kwenye ardhi ambayo ni muhimu sana kwenye kutafuta maji ardhini , kutokana na mipasuko hii au nyufa ambazo ni chanzo kikubwa cha kupenyesha maji na kuhifadhi chini ya ardhi.Mbali na maji , mipasuko hii inaweza kuwa ni mikondo ya kuhifadhi madini ambayo kitalaam inajulikana kama structurally controlled minerals.

Uwasilishaji wa taarifa umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Madini jijini Dodoma na kuudhuriwa na watalaam mbalimbali kutoka taasisi za utafiti za Korea na taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Picha mbalimbali zikionesha katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila na Kaimu Mtendaji Mkuu wa taasisi ya jiolojia na utafiti wa madini Tanzania (GST) pamoja na watendaji wa wizara ya GST, wakipokea taarifa hiyo.