Mnamo tarehe 21/03/2019 majira ya saa 6:15 mchana kumetokea tetemeko la ardhi katika maeneo ya ziwa Rukwa. Taarifa zilizokusanywa na kuchakatwa kutoka kwenye kituo cha kuratibu matetemeko ya ardhi kilichopo Dodoma katika ofisi za Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), zinaonesha kuwa tetemeko hilo lina ukubwa wa 5.1 katika kipimo cha Ritcher. Kitovu cha tetemeko hilo  kipo umbali wa kilometa 40 Kaskazini – Mashariki ya mji wa Sumbawanga, Mkoani Rukwa kwenye latitude 7.82°S na longitude 31.95°E.  Eneo hili lipo katika ukanda wa bonde la ufa la Afrika Mashariki, mkondo wa Magharibi ambao ni njia kubwa ya matetemeko ya ardhi.

Kwa taarifa tulizozipata kutoka kwa mashuhuda mbalimbali, tetemeko hili limesikika katika maeneo ya miji ya Sumbawanga, Chunya, Jiji la Mbeya, Mpanda na sehemu ya mkoa wa Songwe.

Ukubwa wa tetemeko hili la ardhi kitaalamu ni tetemeko linaloweza kuwafanya watu waliolisikia kukimbia kwa hofu toka nje ya majengo, kusababisha uharibifu wa majengo kutegemeana na ubora wa majengo hayo. Pia ni ukubwa unaoweza kusikika na waendeshaji wa vyombo vya moto.

Hadi wakati wa uandishi wa taarifa hii, GST haijapokea taarifa yoyote ya kutokea kwa madhara makubwa kutokana na tetemeko hilo.

GST inaendelea kuwatahadharisha wananchi juu ya kuzingatia ujenzi wa nyumba imara zinazoweza kukabiliana na athari za matetemeko ya ardhi ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza. Pia wananchi wanaombwa kuacha kutaharuki wakati wa tetemeko kwa kukimbia kwani inaweza kusababisha madhara mengine ya kuumizana na kupata mshtuko.

Imetolewa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania

21/03/2019