Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila amesema Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) inazo fursa nyingi ambazo zingeweza kuifanya kuwa Taasisi inayoingiza mapato makubwa.

Prof. Msanjila ameyasema hayo leo wakati wa ziara yake katika taasisi hiyo iliyolenga kujifunza namna GST inavyotekeleza majukumu yake, kufahamiana na watumishi wa taasisi hiyo na kufahamu changamoto zinazoikabili.

Kutokana na fursa za kibiashara zilizopo katika taasisi hiyo, Prof. Msanjila ameishauri kujikita katika kutoa huduma za kibiashara kutokana na uwezo iliyonayo na huduma inayotoa kwa jamii hususan wadau wa Sekta ya Madini nchini.

Amesema umuhimu wa GST bado haujatumika katika namna inavyotakiwa na kueleza kuwa, kutokana na Mabadiliko yaliyofanyika katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, yamelenga kuipa uzito taasisi hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akiangalia sampuli za madini kupitia darubini ndani ya Maabara ya Utafiti wa Madini katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST). Katibu Mkuu amefanya ziara GST ya kuangalia kazi mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo.

Pia, Prof. Msanjila amewataka watumishi wa GST kuwa na udhubutu na kila mmoja kuwajibika kikamilifu katika eneo lake analofanyia kazi na pindi wanapohitaji mwongozo kutoka wizarani, wasisite kufanya hivyo.

Katika hatua nyingine, Prof. Msanjila ameipongeza taasisi hiyo kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu yake na kuongeza kuwa, Wizara ya Madini imepata sifa kubwa kutokana na namna GST ilivyotekeleza majukumu yake kikamilifu.

“ Taasisi yenu imechangia sana kwenye sifa ilizopata wizara wakati wa uwasilishaji wa Bajeti yake mwezi Mei, nawapongeza sana kwa utendaji kazi, matokeo yenu tunayaona,” amesisitiza Prof. Msanjila.

Vilevile, ameishukuru kutokana na namna ambavyo imekuwa ikitoa ushirikiano kwa wizara na kusema kuwa, “ kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati ya wizara na taasisi. Mimi, Waziri na Naibu Mawaziri tunashukuru,”

Akizungumzia suala la kuwaendeleza watumishi, amesema kuwa, wizara imedhamiria kuhakikisha kwamba watumishi wanajiendeleza kielimu na kuongeza kuwa, tayari imeanza mchakato ili watumishi waweze kupata nafasi za ufadhili wa masomo katika fani mbalimbali.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akizungumza na Watumishi wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) baada ya kutembelea kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo.

“Tunakamilisha suala la kupata ufadhili. Wenye nia ya kusoma nafasi zitakuwepo. Binafsi napenda sana watu waende shule na hasa vijana,” amesema Prof. Msanjila.

Katika ziara hiyo, Prof. Msanjila ametembelea Idara mbalimbali za GST ikiwemo maabara mbalimbali za utambuzi wa madini na utengenezaji wa ramani mbalimbali za madini.

Awali, Prof. Msanjila alifanya kikao na Menejimenti ya GST, pamoja na kuzungumza na watuishi wa taasisi hiyo. Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu ameambatana na Mkurugenzi wa Utawala na RasilimaliWatu, Issa Nchasi.

Imeandaliwa na;

Asteria Muhozya na Samwel Mtuwa, Dodoma