TAARIFA KWA UMMA KUHUSU TETEMEKO LA ARDHI LILILOTOKEA MKOANI DODOMA TAREHE 13/07/2016

Leo tarehe 13/7/2016 majira ya saa 12:01:15 asubuhi kumetokea tetemeko la ardhi Mkoani Dodoma ambalo lilikuwa na ukubwa wa 5.1 katika kipimo cha Richter. Kitovu cha tetemeko hilo kipo kiasi cha kilomita 11 mashariki ya mji wa Haneti ambao uko umbali wa kilomita 79 kaskazini mashariki mwa mji wa Dodoma.
Eneo hilo lipo katika ukanda wa bonde la ufa la Afrika Mashariki mkondo wa mashariki. Maeneo ya ukanda wa bonde la ufa hukumbwa na matukio ya matetemeko ya ardhi mara kwa mara hii ni kutokana na ukweli kwamba tabaka la miamba katika maeneo hayo lina kina kidogo ikilinganishwa na maeneo ambayo yako nje ya ukanda wa bonde la ufa. Hali hii husababisha matabaka ya miamba katika ukanda huo kuwa katika hali ya fukuto jingi la joto na kusigana kwa miamba ambapo husababisha miamba hiyo kukatika hali ambayo husababisha mtikisiko wa ardhi ambao ndio huitwa tetemeko la ardhi.
Hadi hivi sasa hakuna taarifa zilizopatikana kuhusu kutokea kwa madhara kuhusiana na tukio hilo. Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) unawashauri wananchi kuchukua tahadhari wakati wote ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea pindi linapotokea tetemeko la ardhi. Wakati wa tukio la tetemeko la ardhi endapo watakuwa ndani ya jengo/nyumba waendelee kubaki humo na wachukue tahadhari kwa kusimama kwenye makutano ya kuta za jengo hadi mitetemo itakapomalizika ndipo watoke nje. Wakiwa nje wasimame mahali pa wazi mbali na nguzo za umeme, nyaya za umeme, majengo marefu pamoja na miti mirefu. Na wale ambao watakuwa nje wakati watukio wanashauriwa kubaki nje wasikimbilie ndani ya majengo na endapo watakuwa wanaendesha vyombo vya moto wanashauriwa wasimame hadi mitetemo itakapotulia.
Baada ya hali kutulia wanashauriwa kukagua majengo/nyumba zao ili kuona kama kumetokea madhara yoyote na ikiwa lazima waombe ushauri wa wataalamu wa majengo ili wakague majengo hayo kuona kama yana usalama.
 GST imepewa majukumu ya kuratibu majanga ya asili ikiwemo matetemeko ya ardhi na imefunga vipimo vya matetemeko katika vituo tisa nchi nzima ambavyo vipo katika maeneo ya Dodoma mjini, Arusha, Babati, Singida, Geita, Kibaya, Kondoa, Mbeya na Mtwara.
Imetolewa na

Mtendaji Mkuu,
Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST)
13/07/2016